Mwanafunzi anayesoma sekondari mkoani Mbeya amekamatwa akiwa na kete za madawa ya kulevya aina ya cocaine eneo la Mbalizi mkoani humo.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya, Dhahir Kidavashari amesema kuwa polisi wamemkamata mwanafunzi huyo akiwa anaziuza dawa hizo kwa watu mbalimbali na kwamba upelelezi wa kuwadaka mapapa unaendelea.
Kukamatwa kwa kijana huyo kunatokea siku moja baada ya Rais John Magufuli kuunga mkono kazi ya Makonda huku akiwaagiza wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama kuwashughulikia wote wanaojihusisha na dawa za kulevya bila kujali huyu ni nani.
Kidavashari amesema kwamba vita dhidi ya dawa za kulevya ilikuwa ikiendelea, lakini sasa imepata msukumo mpya ambao unalenga kuukata mnyororo mzima wa mtandao unasambaza dawa hizo.
Mapema Jumatatu hii Rais Magufuli alimuunga mkono Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na jitihada zake dhidi ya biashara hiyo haramu huku akiagiza jeshi la polisi kuwashughulikia wale wote wanaojihusisha na madawa ya kulevya bila kujali wadhifa wao.
Source: Global Publishers