Jiji la Lagos nchini Nigeria limepitisha sheria ya kuwanyonga hadi kufa watu watakaokamatwa na hatia ya kuwateka watu na kudai malipo.
Sheria hiyo mpya ambayo tayari imesainiwa na gavana wa jimbo hilo Akinwunmi Ambode, imeweka hukumu ya kuuawa kwa watekaji watakapatikana na hatia ya mateka kufia mikononi mwao.
Pia sheria hiyo imeweka wazi adhabu ya kifungo cha maisha gerezani kwa watekaji wanaodai malipo ili kuwaachia mateka wao.
Serikali ya jimbo hilo imedai kuwa vitendo vya utekaji watu na kudai malipo umefikia hatua ambayo lazima pawepo sheria kali za kuukomesha.
Utekaji nchini Nigeria umefikia katika hatua ya kutishia usalama wa raia wa kawaida huku mwezi Oktoba mwaka jana wanafunzi wanne, makamu mkuu wa chuo na baadhi ya walimu wa shule ya Lagos Model School, Epe, wakitekwa.