Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf ameamrisha kuzuia safari za viongozi wa serikali kusafiri nja ya nchi kwa siku 60 kuanzia mwezi wa Februari.
Taarifa iliyotolewa na ofisi yake siku ya Jumamosi imewataja waathirika wa agizo hilo kuwa ni mawaziri wote, wakuu wote wa tume na taasisi za serikali pamoja na wasaidizi wao.
Hata hivyo rais Sirleaf yuko tayari kutoa ruhusa maalum kwa kiongozi yeyote kati ya waliotajwa ingawa ruhusa hiyo itatolewa baada ya mazungumzo ya ana kwa ana na yeye.
Kwa namna moja au nyingine viongozi kadhaa wa Afrika wanaonekana kuendelea kuiga utaratibu wa rais wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli.
Rais Sirleaf ameweka wazi kuwa mazungumzo ya ana kwa ana na kiongozi wa serikali atakayetaka kusafiri nje yatalenga kuhakikisha endapo safari hiyo ina manufaa kwa taifa na ina hoja za msingi za kuhalalishwa.
Ingawa taarifa hiyo haikueleza sababu zilizopelekea kufikiwa kwa hatua hiyo lakini wadadisi wa mambo wanadai kuwa hazina ya fedha za kigeni nchini humo imeishiwa.