Mchoro huo japo uko mgongoni mwake uliuzwa na ukanunuliwa na mkusanyaji sanaa kutoka Ujerumani, Rik Reinking.
Tena, kuna makubaliano- kwamba Steiner atakuwa akikaa mgongo wazi kwenye maonyesho akinadi mchoro huo, na hatimae Steiner atakapofariki basi ngozi yake itatundikwa kwenye fremu kwa ajili ya maonyesho zaidi.
Steiner mwenyewe aliwahi kufanya kazi kama meneja wa duka la uchoraji tattoo huko Zurich lakini mpango huo wote ulifanikishwa na rafikie wa kike ambae ndiye aliyemfahamisha kwa mchoraji huyo wa ubelgiji Wim Delvoye, aliyekuwa akitafuta mtu ili atekeleze wazo lake hilo tata la kumchora mtu tatoo mgongo mzima kwa ajili ya kuiuza.
Delvoye alikuwa akifahamika vyema kwa mtindo wake mwengine tata wa kuchora tatoo kwenye migongo ya nguruwe.
Mchoro huo ulichukua saa 40 kumalizika- na unajumisha vitu vya kawaida kama maua aina ya waridi na mengineyo , samaki wanaopatikana sana huko Uchina waitwao koi, picha za watoto, mchoro wa mwanamke anaefanana na Madona lakini pia mchoro ulio na utata zaidi wa fuvu la kichwa cha mwanadamu.