Muswada wa Sheria ya Madaktari, Madaktari wa Meno na Wataalamu wa Afya Shirikishi wa Mwaka 2016 umeondolewa Bungeni na Serikali.

Naibu Spika, Dk Tulia Ackson amesema serikali imeamua kuuondoa muswada huo kwa sasa mpanga utakapopangwa tena.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kigwangalla alisema serikali imeuondoa muswada huo kutokana na wadau wa sekta ya afya kutoridhika kwamba hawajatendewa haki.

Amesema japo wadau hao, waganga wasaidizi na waganga wasaidizi wa meno, walishirikishwa katika kutoa maoni kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, inaonekana hawajaridhika kutokana na kitendo cha kutoingizwa rasmi kwenye jina la muswada huo, kitendo ambacho wanaona ni kama dalili za kuondolewa kazini kama ungepitishwa.

Amesema hakuna anayekataa kwamba hao ni wataalamu muhimu katika sekta ya afya, isipokuwa hawawezi kutambuliwa kama madaktari kutokana na ukweli kwamba mtu anatambuliwa kuwa daktari kama ana shahada ya kwanza, sio chini ya hapo.

Amesema kitaaluma, daktari na daktari msaidizi ni watu wawili tofauti, kwani mtu akitaka kusoma udaktari lazima asome miaka mitano zaidi ya ile elimu ya elimu ya stashahada anayosoma daktari msaidizi, hivyo si halali wakaitwa madaktari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *