Mwanamuziki wa Bongo fleva, Rehema Chalamila ‘Ray C’, amesema kwamba yupo mbioni kurudi upya katika muziki wa ushindani kwa kuwa anaamini bado muziki wake una mashabiki wa kutosha.
Ray C amesema hayo baada ya kumaliza kutumbuiza nyimbo zake katika kikao cha Kamati ya Ushauri cha Mkoa wa Dodoma (RCC kilichohudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa.
Mara baada ya kupanda jukwaani, Ray C alianza kuimba nyimbo zake za zamani huku vingozi mbalimbali wakijumuika naye kwa kucheza.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Dodoma, Paulo Luhamo na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Dodoma kupitia CCM, Felister Bura, walikuwa miongoni mwa walioanza kumuunga mkono Ray C kwa kujumuika naye na kucheza pamoja.
Wengine waliocheza na Ray C ni mfanyabiashara maarufu Tanzania, Haidari Gulamali, kisha Ray C alikwenda katika jukwaa kuu na kumpa mkono Waziri Mkuu Majaliwa, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana na Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenister Mhagama.
Kwa upande mwingine Ray C amesema kwamba kwa sasa ameshaachana na matumizi ya dawa za kulevya na lengo lake kubwa ni kurudi katika biashara yake ya muziki kutokana na kuendelea kukubalika kwa nyimbo zake.