Watu 13 wamekamatwa wakiwemo wakulima  na  wafugaji  wilayani Malinyi  kutokana na kukaidi agizo la serikali la kusitisha shughuli za kibinadamu katika bonde la mto Kilombero mkoani Morogoro.

Kamati ya Ulinzi na Usalama ikiongozwa na mkuu wa mkoa wa Morogoro Kebwe Steven Kebwe imewakamata watu hao pamoja na  matrekta sita  na gari moja  mara baada ya kutembelea eneo hilo maalum lililotengwa na serikali na kukuta watu hao wakiendelea   kufanya shughuli  za  kibinadamu ikiwemo  kilimo, ufugaji  na  uvuvi haramu.

Eneo  hilo hifadhi ya bonde la mto Kilombero limetengwa na serikali kwa ajili ya hifadhi mwaka 2012, lakini bado jitihada hizo hazikuleta mafanikio baada ya baadhi ya wananchi kurudi katika eneo hilo na kuendelea kufanya  shughuli za kibinadamu ndani ya eneo la kinga.

Kulingana na hali hyo Dkt. Kebwe amezitaka Halmashauri za Wilaya tatu za kilombero, Ulanga na Malinyi ambazo zinapakana na mto huo kufanya ufuatiliaji wa karibu katika kuhifadhi bonde hilo.

Mkuu wa mkoa huyo amesema kuwa  zoezi hilo la kamata kamata katika bonde  la mto kilombero litakuwa endelevu na matrecta yaliyokamatwa yatapelekwa kituo cha polisi na wamiliki wa zana hizo wataitwa ili kujibu tuhuma zinazowakabili za kufanya shughuli za kilimo katika eneo hilo ambalo limepigwa marufuku.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *