Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Akinwumi Adesina amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli huku akiahidi kuwa benki hiyo itaizalishia Tanzania umeme wa gharama nafuu.
Mazungumzo hayo yamefanyika nchini Ethiopia,ambako Rais Magufuli amehudhuria mkutano wa 28 wa wakuu wa nchi za Afrika ambapo amemshukuru kwa ushirikiano mzuri ambao Tanzania inaupata kutoka Benki hiyo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Pia Rais Magufuli amemuomba Rais huyo wa AfDB kuendeleza na kuongeza zaidi ushirikiano huo hasa katika maeneo ya kipaumbele ambayo Tanzania inayatekeleza hivi sasa.
Kwa upande wake Bw. Akinwumi Adesina amesema Benki hiyoitaendeleza ushirikiano na uhusiano wake na Tanzania na kwamba Tanzania itanufaika kupitia vipaumbele vipya vya AfDB viitwavyo “Hi 5” vinavyohusisha uwezeshaji miradi ya uzalishaji wa nishati, ujenzi wa viwanda, uzalishaji wa chakula, miundombinu ya kuunganisha nchi na nchi na kuboresha maisha ya watu.
Pia Bw. Akinwumi Adesina amekubali ombi la Rais Magufuli la kuitaka AfDB kushirikiana na Tanzania kupata suluhisho la kuzalisha umeme mwingi na wa gharama nafuu na ameahidi kumtuma Makamu wa Rais wa AfDB anayeshughulikia masuala ya nishati kuja Tanzania haraka iwezekanavyo ili kuanza utekelezaji wa ombi hilo.