Ligi kuu Uingereza jana imeendelea kwa michezo saba katika viwanja tofauti huku macho na masikio ya watu yakiwa katika uwanja wa Anfield ambapo Liverpool iliwaalika viongozi wa ligi hiyo timu ya Chelsea.

Katika mechi hiyo iliyoanza majira ya saa tano kamili usiku kwa saa za Afrika Mashariki ilishuhudiwa kwa kumalizika kwa sare ya 1-1.

Mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika Chelsea walikuwa wanaongoza huku goli lao likiwekwa kimiani na beki wake David Luiz katika dakika 24 ya mchezo huo baada ya kupiga faulo iliyomshinda mlinda mlango wa liverpool, Simon Mignolet.

Kipindi cha pili Liverpool walionekana kubadilika mpaka kupelekea kusawazisha goli kupitia mshambuliaji wao Georginio Wijnaldum katika dakika 57 ya mchezo baada ya kuunganisha krosi kwa kichwa.

Katika mechi nyingine Arsenal wameshindwa kutamba katika uwanja wa nyumbani baada ya kukubali kichapo cha goli 2-1 kutoka kwa Watford.

Ligi hiyo inaendelea tena leo kwa michezo mitatu katika viwanja tofauti Manchester United wakicheza na Hull City katika Uwanja wa Old Trafford, Westham United watawakaribisha Macnhester Ciy katika uwanja wa Upton Park na Stoke City watacheza na Everton katika uwanja wa Britania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *