Jumla ya tani 35,491 za chakula zinahitajika ili kukabiliana na hali ya upungufu wa chakula na lishe kati ya mwezi Februari na mwezi Aprili mwaka huu unaowakabili watu 1,186,028.
Taarifa hiyo ya serikali imetolewa bungeni leo na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Tizeba wakati akitoa kauli ya serikali kuhusu hali ya upatikanaji wa chakula nchini huku akisisitiza kuwa hali ya upatikanaji wa chakula nchini bado ni wa kuridhisha pamoja na kuwa baadhi ya maeneo yenye upungufu wa chakula.
Tizeba amesema taarifa hiyo ni kwa mujibu wa matokeo ya tathmini ya serikali iliyobaini kupungufu huo katika halmashauri 55 nchi nzima.
Aidha amesema kuwa jumla ya watu 118,603 wasio na uwezo wa kupata chakula watahitaji tani 3,549 za chakula cha bei nafuu kwa haraka na tayari serikali imeanza kuchukua hatua za kushusha bei ili wananchi waweze kumudu bei zake.
Amesema kutokana na kuchelewa kwa mvua na mtawanyiko usioridhisha katika maeneo mengi nchini athari zinazotarajiwa kutokea ni pamoja na matarajio ya malengo ya uzalishaji wa mazao ya chakula huenda yasifikiwe, uzalishaji wa mbegu za mazao ya kilimo utapungua, uwezekano wa kuongezeka kwa bei za baadhi ya mazao ya chakula upo, kupungua kwa mapato yatokanayo na ushuru wa mazao kwa baadhi ya halmashauri.