Majeshi ya maalum ya usalama ya Ecowas yaliyopo nchini Gambia, yamemkamata mkuu wa majeshi ya nchi hiyo aliyekuwa akiongoza vikosi wakati wa utawala wa rais Yahya Jammeh.
Majeshi hayo pia yamedai kukamata silaha kwenye makazi binafsi ya rais Jammeh ambaye ameondoka nchini humo kufuatia mgogoro wa kisiasa uliotishia kutokea kwa machafuko.
Msemaji wa vikosi hivyo vya Ecowas, Jen. Francois Ndiaye amethibitisha kutokea kwa matukio yote mawili huku akikataa kutoa ufafanuzi wa sababu za kumkata mkuu huyo wa majeshi.
Jen. Bora Colley, aliyekuwa mkuu wa kikosi maalum cha makomando alikamatwa akiwa nchini Senegal huku kukiwa hakuna taarifa za mahali alikopelekwa.
Vikosi hivyo pia vinadai kuivamia nyumba ya makazi binafsi ya rais Jammeh iliyopo kwenye kijiji cha Kanilai na kukuta bunduki na milipuko.
Jen. Colley pia alikuwa ndie mkuu wa kambi ya kijeshi iliyopo Kanilai, ambapo kwa mujibu wa gazeti la Freedom rais Jammeh alikuwa amepanga kwenda na kustaafu kabla ya kubadili mawazo na kupinga matokeo kisha kulazimishwa kuihama nchi hiyo.
Kwa mujibu wa Jen. Gerrie Nel walinzi wanne wa mke wa rais Jammeh nao pia wamekamatwa kwenye mpaka wa Karang nchini Senegal.