Umoja wa Mataifa (UN) umesema kuwa utaendelea kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya Umoja huo na Tanzania.
Katika maongezi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres na Rais John Magufuli wamekubaliana kuimarisha ushirikiano wake na Tanzania katika kutekeleza majukumu mbalimbali, hususan tatizo la wakimbizi.
Guterres amesema hayo jana, alipokutana na Rais Magufuli kando ya Mkutano wa 28 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU), unaoendelea mjini Addis Ababa nchini Ethiopia.
Guterres aliahidi kuwa UN itaongeza ushirikiano na Tanzania na kwamba itatia msisitizo zaidi katika kukuza wadau mbalimbali wa maendeleo ndani ya jumuiya ya kimataifa, kuchangia juhudi zinazofanywa na Tanzania katika kuwapa hifadhi wakimbizi wa nchi mbalimbali tangu mwaka 1971.
Kwa upande wake, Rais Magufuli alimpongeza Guterres kwa kuchaguliwa kwake hivi karibuni kushika wadhifa huo.
Amesema Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na Umoja wa Mataifa. Rais Magufuli pia alimweleza Katibu Mkuu huyo wa UN juhudi mbalimbali, zinazofanywa na Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki, kushughulikia mgogoro wa Burundi chini ya Mpatanishi wa mgogoro huo, Rais mstaafu Benjamin Mkapa na alimhakikishia kuwa juhudi hizo zinakwenda vizuri.