Rais wa Marekani, Donald Trump amemfukuza kazi kaimu mwanasheria mkuu, Sally Yates baada ya kupinga kauli ya Trump ya kuwawekea vikwazo raia wanaotoka baadhi ya nchi za kiislamu.
Kaimu mwanasheria huyo aliwaagiza mawakili wa idara ya haki nchini humo kutotetea uamuzi wa kuwawekea vikwazo raia wanaotoka katika baadhi ya mataifa ya kiislamu.
Taarifa ya Ikulu ya Whitehouse imemshtumu kwa usaliti aliokuwa anaufanya wa kumpinga rais kutokana na sheria zake.
Sally Yates ambaye aliteuliwa na Obama amesema kuwa hafikirii kwamba katazo hilo ya muda kwa raia wa mataifa saba ya Kiislamu ni halali.
Wadhfa wake umechukuliwa na kiongozi wa mashtaka katika mahakama ya kijimbo huko Virginia Dana Boente.
Agizo hilo la rais lililotiwa saini Ijumaa iliopita limesababisha maandamano nchini Marekani na ughaibuni.
Awali kundi moja la wanadiplomasia liliandika barua likikosoa agizo hilo wakisema litazidi kuhatarisha usalama wa taifa hilo.