Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli amewashukuru viongozi wote wa Umoja wa Afrika (AU) kwa kuamua jengo la umoja huo kuitwa jina la Mwalimu Julius Nyerere.
Magufuli amesema kuwa sababu ya kupewa jina la mwalimu ni kutambua mchango wake katika kupigania amani na usalama na alibainisha kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa Mwafrika halisi na kiongozi mahiri na shupavu.
“Na kwa hakika naweza kusema kuwa alikuwa mmoja wa viongozi bora kabisa ambaye amewahi kutokea katika Bara letu, katika maisha yake yote Mwalimu Nyerere alipambana ili kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa Afrika, alikuwa mmoja wa waanzilishi wa umoja huu, sisi Watanzania kwa hakika tunajivunia sana Mwalimu Nyerere kuwa Baba wa Taifa,” alisema Dk Magufuli.
Dk Magufuli aliongeza kuwa Mwalimu Nyerere alitoa mchango mkubwa katika kupambana na ubaguzi na unyonyaji wa kila aina, alisaidia ukombozi wa nchi nyingi za Afrika, na hata alipong’atuka katika hatamu za uongozi wa Taifa la Tanzania aliendelea kutoa mchango wake kupigania amani katika nchi za Afrika.
“Wito wangu kwenu, waheshimiwa viongozi ni kwamba, sambamba na kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa jengo hili, itakuwa ni jambo jema zaidi kama tutajitahidi kufuata nyayo zake pamoja na kuishi maisha ya viongozi wengine hodari wa Bara hili wakiwemo Kwame Nkrumah, Ahmed Ben Bella, Sekou Toure, Gamal Abdel Nasser na bila kusahau shujaa wetu mwingine Nelson Mandela,” alisisitiza Rais Magufuli.