Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad amesema kuwa mgogoro wa Zanzibar wa siasa visiwani humo utamalizika endapo viongozi wa vyama vyote wa siasa watakaa chini pamoja na kufanya mazungumzo.
Maalim Seif amesema jambo la muhimu ni viongozi kukubali Zanzibar kuna tatizo alafu mambo mengine yafuate.
Amesema anaamini kama kuna nia njema, maridhiano yanaweza kupatikana Zanzibar na migogoro yote ya kisiasa kumalizika.
Amesema Serikali iliyopita ya Umoja wa Kitaifa, ilikuwa na mafanikio makubwa na kwamba anavyoona hakuna kitakachorudisha hali ile, kama si kwa vyama kushirikiana.
Aidha, Maalim Seif alisema anajua kuna majaribio makubwa yanafanywa kutafuta ufumbuzi, hivyo ufumbuzi ni vema upatikane ili kuridhisha pande zote, na kwamba kuna njia nyingi ya kupata muafaka na hiyo ni pamoja na kufanyika mazungumzo, lakini ni baada ya kila upande kukubali kuwa Zanzibar kuna tatizo.
Akizungumzia kugombea tena nafasi ya urais mwaka 2020, Maalim Seif alisema ni vema kusubiri ili kuona hali ya kisiasa itakapofika wakati huo.
Akizungumzia mgogoro ndani ya CUF, Hamad amesema Msajili wa Vyama vya Siasa aliruhusu upande wa Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba kuchukua Sh milioni 369 ambazo ni fedha za ruzuku na kwamba baadaye chama kitashindwa kuzijibia matumizi yake.
Source: Habri Leo