Mahakama ya Kenya imetoa amri kwa idaya ya uhamiaji ya nchi hiyo kuhakikisha kuwa wanachama wawili wa upinzani nchini Sudani Kusini waliopotea kwa siku nne sasa hawarudishwi nchini kwao bila kufuata utaratibu rasmi.
Watu hao Dong Samuel na Aggrey Idris wanadaiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha huku polisi wa idara ya uhamiaji ikikanusha kuwashikilia mahabusu watu hao.
Kwenye mahakama hiyo ambayo ilijaa ndugu wa watu hao waliokuwa wakitaka kufahamu hatma ya kupatikana kwa ndugu zao, jaji kiongozi wa kesi hiyo Luka Kimaru alisema:
- Kitengo cha upelelezi wa makosa ya jinai cha polisi kinapaswa kufungua shauri la kutafuta watu hao walipo
- Kampuni ya mawasiliano ya Safaricom inapaswa kutoa taarifa ya mawasilino ya mwisho ya wawili hao
- Mkuu wa idara ya uhamiaji hapaswi kuwarudisha nchini mwao watu hao bila kufuata taratibu rasmi za uhamiaji
Mke wa hayati, John Garang muasisi na rais wa kwanza wa taifa hilo, Rebecca Garang, tamesema kuwa ameshangazwa na kile kilichotokea kwa watu hao.
Rebecca Garang amesema kuwa ilimpasa mtoto wake kuondoka Kenya baada ya kutajwa kwenye orodha ya watu 16 wanaohusishwa na upinzani ambao walikuwa wanatakiwa na serikali ya Sudani Kusini.
Novemba mwaka jana Serikali ya Kenya ilimrudisha Sudani Kusini aliyekuwa msemaji wa kambi ya upinzani, James Gatdet kwa kilichodaiwa kuwa ni kusherehea hatua ya Umoja wa Mataifa kumfuta kazi kamanda wa jeshi la Kenya aliyekuwa akiongoza vikosi vya ulinzi na usalama nchini Sudani Kusini kisha akatuhumiwa kuzembea hatari zilizokuwa zikiwakabili wananchi wa nchi hiyo na kusababisha mauaji ya mamia ya raia.
Mkuu wa kambi ya upinzani na makamu wa zamani wa rais, Riek Machar alipinga hatua hiyo ya serikali ya Kenya.