Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameishukuru Serikali ya India kwa ufadhili wake wa miradi ya maji katika miji 17 nchi ambayo inalenga kupunguza tatizo la maji kwa wananchi wengi nchini.

Makamu wa Rais ametoa kauli hiyo Jijini Dar es Salaam katika hafla ya Maadhimisho ya miaka 68 ya Siku ya Kitaifa ya Jamhuri ya India sherehe ambazo zimeambatana na uzinduzi rasmi wa majengo ya ofisi mpya ya ubalozi wa India hapa nchini.

Makamu wa Rais pia ameishukuru Serikali ya India kwa msaada wake wa shilingi milioni 500 alioutoa kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera ambao walikumbwa na tetemeko la ardhi mwaka jana.

Samia pia ametoa salamu za rambirambi kwa Serikali ya India kufuatia ajali ya treni iliyotokea katika Jimbo la Andhra Pradesh na kusababisha vifo vya watu 30 na kujeruhi wengine.

Kwa upande wake, Balozi wa India hapa nchini Sandeep Arya amemhakikishia Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Serikali ya India itaendelea kudumisha na kuendeleza mahusiano mazuri yaliyopo kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa pande zote Mbili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *