Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema kuwa wizara hiyo itahamia Dodoma ndani ya siku 14 zijazo ili kutekeleza agizo la Rais John Pombe Magufuli la Serikali kuhamia Dodoma kabla ya 2020.

Ummy Mwalimu amethibitisha kwamba ofisi ya waziri, naibu waziri na Katibu Mkuu wake wa wizara, hazitabaki Dar es Salaam bali zitakuwa Dodoma.

Kuhamia kwa wizara hiyo Dodoma, itakuwa ni wizara ya tano, uhamisho huyo ulitanguliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyehamia Septemba mwaka jana na baadaye akafuata Waziri wa Nchi katika ofisi yake, Jenista Mhagama anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu.

Mawaziri wengine waliohamia Dodoma ni wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene na msaidizi wake, Selemani Jafo pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki.

Kutokana na ratiba iliyotangazwa na Waziri Mkuu mwaka jana, waziri mkuu na mawaziri wote pamoja na makatibu wakuu wa wizara, wanatakiwa kuwa tayari wamehamia Dodoma kufikia Februari 28, mwaka huu.

Ratiba hiyo inaonesha kati ya Machi na Agosti mwaka huu, watendaji wa wizara wanatakiwa kupanga na kutenga bajeti kwa maofisa wao kuhamia makao makuu ya nchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *