Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, anatarajiwa kuongoza matembezi ya Wiki ya Sheria kuanzia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu hadi  viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, Januari 29 mwaka huu.

Katika matembezi hayo Mwinyi atazindua rasmi maadhimisho ya Wiki ya Elimu ya Sheria ikiwa ni sehemu ya sherehe za kuelekea maadhimisho ya kilele cha Siku ya Sheria nchini ambapo pia katika mikoa yote ya Tanzania wananchi wataweza kupata fursa ya kujua sheria katika sehemu maalum zitakazokuwa zimeandaliwa.

Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania  Prof. Ibrahim Hamis Juma  amesema mahakama itawaelimisha wananchi jitihada mbalimbali ilizochukua zenye lengo la kuboresha huduma zake kupitia mpango-mkakati wa miaka mitano inaoutekeleza katika kutoa haki kwa wakati na kuwezesha ukuaji wa uchumi.  Haya yatafanyika kwenye mabanda yatakayokuwepo kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja kabla ya kilele chake.

Jaji Juma ametoa rai kwa wananchi kutembelea sehemu zote zilizoandaliwa kwa ajili ya utoaji elimu ya sheria nchini kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali na kupata huduma  za kisheria

Miongoni mwa  huduma zitakazotolewa katika wiki hiyo  ni pamoja na taratibu za ufunguaji mashauri katika ngazi mbalimbali za mahakama, taratibu za kesi za dhamana, taratibu za rufaa,  taratibu za kesi za mirathi, ndoa na talaka, taratibu za kupokea na kushughulikia malalamiko na msaada wa kisheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *