Utata mkubwa umeibuka nchini Sierra Leone baada ya mamilioni ya Dola za Marekani zilizotolewa msaada kwaajili ya kupambana na ugonjwa wa Ebola kupotea katika mazingira ya kutatanisha.
Ikiwa sasa ni takribani miaka mitatu tangu nchi hiyo ikumbwe na ugonjwa huo ulioua zaidi ya watu 4,000 bado kuna maswali juu ya wapi zilipotumika $14m (TZS 31bn).
Ripoti ya ukaguzi wa ndani wa fedha uliofanywa na mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali wa nchi hiyo, Bi. Taylor-Pearce imeonyesha kukosekana kwa maelezo ya kutosha ya ufafanuzi wa namna kiasi hicho cha pesa kilivyotumika.
Pia mkaguzi huyo amedai kuwa hakuna ushahidi wa kuthibitisha kuwa kulifanyika malipo ya $4m (TZS 9bn) kwa wafanyakazi waliokuwa kwenye hatari zaidi ya kuambukizwa maradhi hayo.
Tangu kuibuka kwa ugonjwa huo nchini humo watu 4,000 walipoteza maisha ambapo miongoni mwao zaidi ya watu 200 walikuwa wauguzi.