Kumeibuka mvutano nchini Marekani kuhusiana na kauli ya msanii Madonna aliyoitoa hivi karibuni kuhusiana na rais mpya wa nchi hiyo Donald Trump.
Wakati akiwa kwenye maandamano ya kumpinga rais huyo yaliyofanyika kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Washington DC yaliyofanyika siku ya Jumamosi, Madonna alikaririwa akisema kuwa alifikiria sana kuilipua ikulu ya nchi hiyo ‘White House’.
Kauli hiyo ambayo ilihamsha hasira za wafuasi wa Trump ambao walidai kungekuwa na vurugu kubwa endapo kauli hiyo ingetolewa dhidi ya mtangulizi wa Trump, Barack Obama.
Hata hivyo msanii huyo wa Pop amesema kuwa kauli yake ‘ilitafsiriwa vibaya’.
‘Mimi si mtu wa vurugu, sihamasishi vurugu na ni muhimu kwa watu kusikiliza na kuielewa hotuba yangu yote na sio kifungu kimoja cha maneno’.
Maneno kamili ya Madonna yanaonyesha kabisa kuwa hakuwa na lengo baya kwenye kauli hiyo na hususani endapo msikilizaji au msomaji atayasikiliza yote.
Kauli kamili ya Madonna ni hii:
‘Yes, I’m angry. Yes, I am outraged. Yes, I have thought an awful lot about blowing up the White House. But I know that this won’t change anything’.
Aliyesababisha kuzuka kwa mabishano kuhusiana na kauli hiyo ni msemaji mpya wa Ikulu ya Marekani Reince Priebus alikiambia kituo cha televisheni cha Fox News: ‘Moja wa waimbaji anasema anatamani kuilipua ikulu. Namaanisha, unaweza kufikiria maneno hayo yangesemwa kuhusu rais Obama?’