Makamu wa zamani wa rais wa Zimbabwe Joice Mujuru ameanza kuonja joto ya jiwe ya kisiasa baada ya chama chake kipya alichokianzisha kuangushwa vibaya na chama tawala cha ZANU-PF kwenye uchaguzi mdogo uliofanyika wiki iliyopita.
Kwenye uchaguzi huo ZANU-PF imefanikiwa kubakisha jimbo la Bikita Magharibi vijijini kwa kupata kura 13,156 dhidi ya kura 2,453 zilizoambuliwa na mgombea wa chama cha Bi. Joice, Zimbabwe People First.
Mujuru ambaye alikuwa makamu wa rais kwa miaka 10, alikuwa akihesabiwa kama mrithi asilia wa rais Mugabe pindi atakapong’atuka madarakani lakini mwaka 2014 wawili hao walikosana na Bi. Joice alifukuzwa kwenye chama hicho kwa madai ya kupanga njama za kumuua kiongozi huyo mkongwe zaidi barani Afrika.
Hata hivyo Bi. Joice alikanusha madai hayo.
Pamoja na kuiongoza nchi hiyo tangu mwaka 1980 na sasa akiwa na miaka 92 tayari rais Mugabe ameshatangaza nia ya kuwania urais kwenye uchaguzi wa mwaka 2018.
Matokeo hayo ya uchaguzi huenda yakaathiri mazungumzo yanayoendelea ya kuunda muungano wa upinzani kwaajili ya kupambana na rais Mugabe kwenye uchaguzi ujao.
Mazungumzo hayo yanayofanywa baina ya chama kikubwa cha upinzani nchini humo cha MDC kinachoongozwa na Morgan Tsvangirai na chama cha Bi. Joice bado hayajafikia muafaka wa namna ya kuunda umoja huo na mgawanyo wa majukumu na madaraka.
MDC walisusia uchaguzi wa Jumamosi kwa madai ya mazingira ya uchaguzi kukipendela chama tawala.