Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amesema ushindi wa CCM wa ubunge na madiwani katika Uchaguzi Mdogo uliofanyika juzi nchini ni ishara ya ushindi wa chama chake katika uchaguzi ujao kutokana na wananchi kuonesha imani kwake na serikali yake.

Rais Magufuli amesema ushindi huo ni kipimo cha utendaji wake kwa wananchi na hivyo umemuongezea ari ya kuwatumikia wananchi kwa moyo wake bila ya kujali changamoto mbalimbali zilizopo.

CCM mbali ya kushinda kiti cha ubunge cha Dimani visiwani Zanzibar, imeshinda kata 18 kati ya kata 19 zilizofanya Uchaguzi Mdogo wa Udiwani juzi kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za kufa kwa waliokuwa wakishikilia nyadhifa hizo na kufutwa kwa matokeo kwa amri ya mahakama.

Kata ambazo CCM imeshinda ni Nyarenanyuki (Arumeru, Arusha), Isegehe (Kahama, Shinyanga), Nkome (Geita), Kiwanja cha Ndege (Manispaa Morogoro), Lembeni (Mwanga, Kilimanjaro), Ihumwa (Dodoma), Matevez (Meru, Arusha), Kimwani (Muleba, Kagera), Igombavanu (Iringa), Kijichi (Mbagala, Dar es Salaam), Ng’hambi (Dodoma), Kinampundu (Singida), Kasansa (Katavi), Malya na Kahumulo (Mwanza), Mkoma (Mara), Misugusugu (Kibaha, Pwani).

CCM imeshindwa katika Kata ya Duru mkoani Manyara, ambako mgombea wa Chadema, Ali Shaaban ameibuka mshindi. Kwa upande wao, baadhi ya wasomi wamesema kwamba chama cha mapinduzi kimeshinda kutokana na kutekeleza ahadi za kuondoa kero za wananchi.

Source: Habari Leo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *