Ratiba ya Serikali kuhamia Dodoma ipo pale pale kwa mawaziri, manaibu, makatibu wakuu wa wizara na manaibu.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama wakati akizungumza na wanahabari mkoani Dodoma jana.
Waziri huyo amesema kuwa hata Waziri Mkuu amekuwa akisisitiza ratiba ya kuhamia Dodoma kwa awamu ya kwanza Februari mwaka huu ambayo itahusisha mawaziri, manaibu mawaziri, makatibu wakuu na manaibu wao na baadhi ya watumishi wa wizara.
Julai mwaka jana, Rais Magufuli alitangaza kuhusu serikali yake kuhamia Dodoma kabla ya kumalizika kwa muhula wake wa kwanza wa miaka mitano.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akihairisha mkutano wa nne wa Bunge la 11 mwaka jana mwishoni alitoa ratiba ya serikali ya ujumla ya kuhamia Dodoma.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alikwisha kuhamia katika makao makuu hayo ya nchi yaliyotangazwa mwaka 1973.