Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto , Ummy Mwalimu amewasilisha Muswada wa Sheria kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, unaolenga kuliwezesha Baraza la Madaktari kuwa huru.

Muswada huo pia unapiga marufuku watu kujiita madaktari ilhali wakifahamu kuwa hawana taaluma hiyo.

Aidha, wadau wa afya leo wanatarajia kutoa maoni yao kwa kamati hiyo kuhusu Muswada wa Sheria ya Madaktari, Madaktari wa Meno na Wataalamu wa Afya Shirikishi wa Mwaka 2016, ambao pamoja na mambo mengine umelenga kuleta nidhamu ya taaluma ya udaktari kutokana na kuwepo na ongezeko la wataalamu wasio na sifa.

Akiwasilisha maelezo ya muswada huo, Ummy alisema sheria hiyo ilikuwa ikihitajika kwa muda mrefu na madaktari ili iendane na mahitaji ya sasa.

Akizungumzia sifa za mtu anayepaswa kuwa daktari, Ummy alisema miongoni mwa mambo muhimu katika muswada huo ni kuweka masharti ya usajili wa madaktari, madaktari wa meno na wataalamu wa afya shirikishi pamoja na kutoa huduma kwa wanataaluma hao.

Amesema katika sheria mpya itakayokuja, itaanzisha Baraza la Madaktari ambalo Mwenyekiti hatakuwa Mganga Mkuu wa Serikali kama ilivyokuwa awali, ili kuliweka huru. Alisema kutakuwa na mtu yeyote ambaye ni daktari, lakini atateuliwa na waziri kutoka kwenye majina yatakayopendekezwa.

Amefafanua kuwa wakati sheria ya sasa ya mwaka 1959 ilipokuwa ikitungwa kulikuwa na Chuo Kikuu kimoja kinachotoa Shahada ya Udaktari, lakini kwa sasa kumekuwepo na ongezeko na kufikia vyuo vikuu vinane ambavyo vinatoa madaktari.

Pia, madaktari wasaidizi walikuwa wakizalishwa 143 kwa mwaka, lakini sasa wamefikia 183 kwa mwaka na kulikuwa na matabibu 300, lakini kwa sasa wamefikia 495.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *