Wasanii wa maigizo na muziki nchini wamepata somo kuhusu masuala ya kodi kutoka mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

TRA imeendelea na mpango mkakati wake wa kuhakikisha inatoa elimu ya kodi na inamfikia kila mdau ili kuwajengea uelewa wa masuala ya kodi na uhiyari wa kuilipa.

Kodi ni kitu muhimu sana katika kukuza uchumi wa nchi na kwamba maana yake ni makato ya lazima ambayo kila mtu mwenye kipato lazima alipe kwa mujibu wa sheria za nchi na si ombi.

Pia kodi ni tozo ambayo inapatikana kutokana na vyanzo vitatu ambavyo ni ajira, biashara pamoja na uwekezaji na kwamba inatozwa kwa mamlaka ya sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004.

Sheria hiyo ya kodi inaunda upya mfumo wa kodi ya mapato kulingana na mahitaji ya kisasa na kubatilisha sheria ya kodi ya mapato ya 1973.

Mafanikio mengi katika nchi mbalimbali zilizoendelea duniani yametokana na makusanyo ya kodi ambapo huiwezesha nchi kuboresha huduma mbalimbali za maendeleo.

TRA iliwafundisha kuhusu Kodi ya Mapato pamoja na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na kwamba kila mtu mwenye kipato anatakiwa kulipa kodi kwa mujibu wa sheria za nchi.

Wasanii ni wadau muhimu katika nchi kutokana na mchango mkubwa katika ulipaji wa kodi na kwamba Serikali inatakiwa kuhakikisha inawatengenezea mazingira mazuri ya ufanyaji wa kazi zao ili waweze kufaidika lakini pia Serikali iweze kupata mapato kutoka kwao.

Lakini pia wasanii wote ambao hawajajisajili wanatakiwa kuhakikisha wanajisajili katika ofisi za TRA kupatiwa Namba ya Utambulisho wa Mlipa Kodi (TIN) na baadaye atakadiriwa kodi anayostahili kulipa kulingana na namna anavyopata mapato yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *