Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amemteua mwanawe Meja Jenerali Muhoozi Kainerugaba, kuwa mshauri mkuu wa rais kuhusu operesheni maalum.
Mke wa Museveni, Janet Kataaha Museveni ni Waziri wa Elimu na Michezo, wadhifa ambao alikabidhiwa Juni mwaka jana.
Jenerali Kainerugaba amekuwa kamanda wa kikosi maalum cha wanajeshi (SFC) chenye jukumu la kutekeleza operesheni maalum za kijeshi.
Kikosi hicho husimamia ulinzi wa rais na kulinda maeneo muhimu kwa serikali Uganda.
Luteni kanali Don Nabaasa amepandishwa cheo na kuwa kanali na akateuliwa kaimu kamanda wa SFC.
Rais Museveni pia amemteua mkuu mpya wa majeshi, Meja Jenerali David Muhoozi ambaye amepandishwa cheo na kuwa jenerali.
Mkuu wa majeshi wa awali, Jenerali Edward Katumba Wamala amehamishwa na kuteuliwa waziri wa ujenzi.
Haki miliki ya picha AP Image caption Meja Jenerali Muhoozi Kainerugaba (kati) amekuwa kamanda wa kikosi maalum Uganda
Kwenye mabadiliko hayo yaliyotangazwa na msemaji wa Majeshi ya Ulinzi ya Uganda (UPDF) Luteni Kanali, Rais Museveni amempandisha afisa mkuu wa majeshi aliyeongoza operesheni ya kushambulia ikulu ya mfalme wa Rwenzururu, magharibi mwa nchi hiyo.