Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari anatarajia kuongoza mazungumzo ya kutatua mgogoro uliopo nchini Gambia baada ya rais wake Yahya Jammeh kukataa kung’oka madarakani licha ya kushindwa kwenye uchaguzi mkuu.
Rais wa Senegal, Macky Sall, Rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf, Makamu Rais wa Sierra Leone Victor Foh na Raia wa zamani wa Ghana John Mahama ni miongoni mwa viongozi watakaohudhuria mazungumzo hayo jijini Abuja nchini Nigeria.
Buhari na Rais wa zamani wa ghana John Mahama pia wamepewa jukumu na Jumuia ya nchi za Afrika Magharibi, Ecowas kuhakikisha usalama wa mshindi wa uchaguzi Adama Barrow, na pia kuhakikisha kuwepo upokezanaji wa amani wa mamlaka tarehe 9 mwezi Januari.
Rais huyo wa Nigeria na viongozi wengine wa nchi za Afrika Magharibi walimtembelea bwana Jammeh mwezi uliopita lakini hawakufanikiwa kumshawishi kuondoka madarakani
Maafisa wa Ecowas wamesema kuwa hatua za kijeshi za kumlazimisha Jammeh kuondoka madarakani zinafanyiwa tathmini.
Mkuu wa majeshi nchini Gambia ametangaza kumuunga mkono bwana Jammeh na ripoti zingine zinasema kuwa amekuwa na mpango wa kuwaajiri mamluki kutoka nchini Liberia na Ivory Coast.