Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameitaka Kampuni ya Tan Coal Energy inayochimba makaa ya mawe katika mgodi wa Ngaka itimize masharti ya mkataba iliouingia na Serikali mwaka 2008.
Kampuni hiyo iliundwa Aprili 3, 2008 na Kampuni tanzu ya Atomic Resources Limited ambayo wakati huo ilikuwa ikijulikana kama Pacific Corporation East Africa (PCEA).
Kwa sasa inaitwa Intra Energy (T) Limited ikiwa na hisa asilimia 70 na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) asilimia 30.
Kwa mujibu wa mkataba huo, Tan Coal ilipaswa kugharamia dola milioni 14.49 za Marekani kwa ujenzi wa barabara na madaraja ili kuwezesha malori makubwa na madogo kufika mgodini na kusomba makaa hayo.
Hivi sasa malori ya kutoka mgodini yanashusha makaa yaliyochimbwa katika eneo lililokodishwa na Tan Coal la Amani Makolo, kilomita 55 kutoka mgodini na malori makubwa yanapakia makaa hayo kutoka eneo hilo jambo linalozidisha gharama za usafirishaji.