Ikulu ya Marekani ‘White House’ imefanya sherehe ya kumuaga rais wa sasa wa Marekani, Barack Obama anayemaliza muda wake januari 20 mwaka huu baada ya kuwa madarakani kwa miaka nane nchini humo.
Rais Obama anatarajia kuachia madaraka hayo januari 20 mwaka huu kwa kumpatia kijiti cha utawala rais mteule, Donald Trump kutokea chama cha Republican baada ya kumshinda Hillary Clinton wa chama cha Democratic kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana.
Katika sherehe hiyo ya kumuaga rais Obama ilihudhuriwa na mastaa kibao wa Muziki na filamu pamoja na michezo mingine wa Marekani waliokuja kumuaga rais huyo mwenye asili ya Afrika baada ya kumaliza uongozi wake.
Miongoni mwa mastaa waliohudhuria ni pamoja na Paul McCartney, Meryl Streep, Pharrell na Solange, Robert De Niro, Common Usher, Wale, John Legend, Bradley Cooper, Magic Johnson, Tom Hanks na Kelly Rowland.
Mastaa hao walipata nafasi ya kuzungumza na rais Obama, kupata chakula pamoja na kupiga picha za kumbu kumbu kwenye sherehe hiyo iliyofanyika maalumu kwa kumuaga rais huyo anayemaliza muda wake.
Rais Obama amechaguliwa kuwa rais wa Marekani mwaka 2008 mpaka sasa anapoachia madaraka hayo baada ya kuiongoza Marekani kwa miaka minane akimrithi aliyekuwa rais wa wakati huyo George W Bush.