Muigizaji mkongwe wa India, Om Puri amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 66 baada ya kupatwa mshtuko wa moyo nyumbani kwake Mumbai leo.
Mkongwe huyo wa filamu nchini India aliigiza kwenye filamu ya kuchekesha ya East is East iliyofanyika nchini Uingereza ambayo ilisimulia kuhusu maisha ya mhamiaji kutoka Pakistan aliyekuwa akizoea maisha kaskazini mwa England.
Om Puri alijulikana sana kwa ustadi na uigizaji wake katika filamu za Kihindi miaka ya 1980 pamoja na filamu za Kiingereza zikiwemo Mahatma Gandhi ya Richard Attenborough.
Mwaka 2004, alitunukiwa nishani ya staha ya OBE kwa mchango wake katika tasnia ya filamu nchini Uingereza.
Muigizaji huyo amezaliwa 1950 jimbo la Haryana, kaskazini mwa India na filamu yake ya kwanza kuigiza ilikuwa ya Ghashiram Kotwal mwaka 1976.
Nchini India, anafahamika kwa filamu maarufu za Ardh Satya, Sadgati, Paar na filamu ya ucheshi ya Jaane Bhi Do Yaaro.