Mkulima na mkazi wa kitongoji cha Upangwani, kijiji cha Dodoma Isanga, Kata ya Masanze, Kilosa mkoani Morogoro ,Augustino Mtitu(35) aliyechomwa mkuki mdomoni ameruhusiwa kutoka hospitali baada ya hali yake kutengamaa.
Madaktari wamesema kuruhusiwa kwa mgonjwa huyo kumetokana na yeye kupona kufuatia kufanyiwa upasuaji mkubwa mara baada ya kupata mkasa huo.
Tukio hilo lililotokea majira ya saa tano asubuhi mwishoni mwa mwaka jana wakati alipokuwa shambani kuzuia vurugu zilizokuwa zimetokea baada ya wafugaji wa jamii ya kimasai kulisha mifugo yao kwenye shamba la maharage na mahindi yaliyopo katika kijiji hicho.
Mganga mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk Frank Jacob amesema kuwa Mtitu ambaye alilazwa wodi namba moja ya wagonjwa wa majeruhi wa ajali katika hospitali hiyo tangu Disemba 25 mwaka jana aliruhusiwa kutoka hospitalini hapo kwenda nyumbani baada ya kupona jeraha lilolotokana na mkuki na kufanyiwa upasuaji mkubwa.
Dk Jacob alimshukuru Mungu na madaktari, wauguzi kuwezesha kufanikisha upasuaji wa mgonjwa huyo uliofanikisha kuondolewa kwa mkuki aliochomwa mdomoni na kutokea upande wa shingoni .
Kwa upande wake Mtitu, alimshukuru Mungu, madaktari, uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Kilosa na wananchi wa kijiji hicho kwa kuwezesha kunusuru maisha yake.