Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ameguswa na hali ya sasa ya mwanamuziki wa hip hop nchini Chid Benz aliyeathirika na matumizi ya dawa za kulevya.
Hivi karibuni waziri huyo alitembelea nyumbani kwa mwanamuziki huyo na kufanya mazungumzo na mama mzazi wa Chid Benz kuhusu hali ya Afya yake inayoondelea kudhohofika kadri siku zinavyokwenda.
Kupitia akaunti yake ya Instagram, Waziri Nchemba ameeleza kusikitishwa na hali ya Chid Benz na kutumia nafasi hiyo kuwataka wale wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya kuacha mara moja kwani serikali ya awamu ya tano imeazimia kupambana nao.
Alichoandika Mwigulu Nchemba kwenye akaunti yake ya Instagram “Nimekutana na kufanya mazungumzo na mama wa msanii Rashid Makwilo “Chid Benz” ambaye kwa sasa amepatwa na tatizo la dawa za kulevya. Inasikitisha na haivumiliki kuona nguvu kazi ya taifa inapotea huku wauzaji wakinufaika kwa pesa haramu. Ifahamike wazi vita ya serikali dhidi ya magenge, wauzaji na wasambazaji wa madawa ya kulevya imeongezeka hasa katika awamu hii ya tano chini ya Mh. Rais J.P. Magufuli, hivyo anayejihusisha kwa namna yoyote ni vyema akaamua kuachana nayo kabla hajakutwa na mkono wa dola.
Mbali ya vyanzo vya taarifa tulivyonavyo, ni wajibu wa kila aliye RAIA MWEMA kutoa taarifa zitakazosaidia kuangamiza biashara haramu ya madawa ya kulevya.
Pia alieongeza kwa kuandika ‘Naishukuru familia ya Chid Benz kwa jitihada wanazozifanya kuhakikisha kijana mwenzetu anarejea katika hali yake ya kawaida.
Unaweza kuimba, unaweza kufanikiwa, unaweza kutatua matatizo yako bila kutumia madawa ya kulevya.
Chid Benz ni mwanamuziki mkongwe nchini aliyejizolea umaarufu katika anga ya muziki wa hip hop kutokana ubora wa nyimbo zake kama vile Dar es Salaam Stand Up na nyingine kibao.