Kesi ya rufaa ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ya kupinga kunyimwa dhamana imeshindikana kusikilizwa leo baada ya upande wa Jamhuri kukata rufaa ya kupinga kuongezwa muda kwa notisi ya rufaa ya Lema.
Baada ya kushindikana kusikilizwa kwa kesi hiyo, Godbless Lema amerejeshwa rumande katika gereza la Kisongo mkoani Arusha.
Mbunge huyo anakabiliwa na kesi ya uchochezi aliyosomewa katika Mahakama ya Wilaya ya Arusha mbele ya Hakimu Mkazi Deusdedit Kamugisha, Novemba 8, mwaka huu na aliwekewa pingamizi na mawakili wa serikali ya kutopata dhamana baada ya hakimu kusema kuwa dhamana iko wazi.
Lema alikamatwa Novemba 2, mwaka huu mkoani Dodoma kwa kosa hilo baada ya kuhutubia katika mikutano ya hadhara katika kata mbalimbali za Jiji la Arusha kuwa ameoteshwa kuwa Rais Magufuli atakufa kabla ya mwaka 2020, hali inayodaiwa kuleta uchochezi kwa wananchi waliomchagua kuwa rais wa nchi.
Kesi ya mbunge huyo inatarajiwa kusikilzwa tena Januari 2, mwakani kesi hiyo itakapotajwa tena.