Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete ameitaka Serikali kutatua na kukomesha migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na wakulima inayoendelea nchini.
Ridhiwani amesema kuwa licha ya kuishauri Serikali bungeni lakini bado waziri mwenye dhamana ameshindwa kutatua changamoto mpaka kupelekea maafa kwa Taifa.
Mbunge huyo amesema hayo baada ya kutokea mapigano baina ya wakulima na wafugaji mkoani Morogoro ambapo mkulima Augustino Mtuti alipigwa mshale mdomoni na kutokea shingoni.
Ridhiwani amesema kuwa aliwahi kuzungumza bungeni kuhusu migogo ya ardhi iliyopo jimboni kwake, ambayo imesababisha baadhi ya wananchi kupigwa, kuvunjwa mgongo na wengine kupigwa na mishale, lakini waliopewa dhamana walidhani ni utani.
Pia amesema mapigano hayo ya migogoro ya ardhi sasa yameanza kushika kasi nchini ambapo awali lilitokea Mvomero mkoani Morogoro na kwamba litaendelea kutokea pangine kama Serikali itashindwa kuweka nguvu ya ziada ya kulishughulikia.
Mbunge huyo ameongeza kwa kusema kuwa kitendo cha kukaa kimya bila ya kutoa uamuzi wowote kinaonyesha wazi kuwa kuna jambo limefichwa.