Rais mteule wa Gambia Adama Barrow amemtaka mtangulizi wake Yahya Jammeh aondoke madarakani kwa mani kama walivyofanya wakoloni wa nchi hiyo, Waingereza mwaka 1965.
Bwana Barrow amedai kuwa hayuko tayari kuongoza taifa ambalo halina amani.
Kauli ya Barrow imekuja siku kadhaa baada ya Umoja wa Ulaya na Ecowas kumtaka Yahya Jammeh kukabidhi madaraka kwa amani pindi muhula wake wa uongozi utakapomalizika tarehe 19 mwezi Januari 2017.
Hata hivyo Jammeh ambaye awali alitangaza kukubali kushindwa kabla ya kubadili kauli na kudai uchaguzi ulikuwa na makosa mengi, amesema kuwa hayuko tayari kung’atuka madarakani kwa shinikizo la Ecowas wala EU na yuko tayari kuilinda nchi yake kwa namna yoyote ile.