Waziri mkuu wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametembelea gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam na kukagua eneo la ujenzi wa makazi ya askari wa Magereza unaotarajiwa kuanza baada ya wiki tatu zijazo.
Akizungumza na askari wa magereza kabla ya kufanya ukaguzi huo jana Waziri Mkuu alisema ziara aliyoifanya , ni ufuatiliaji wa maagizo ya Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli aliyoitoa wakati alipoenda kukagua gereza hilo.
Waziri Mkuu alisema amefarijika kukuta Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wako eneo la kazi na wameanza kusafisha eneo hilo.
Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua mchango uliofanywa na Serikali ya awamu ya nne katika suala la makazi ya askari kama vile wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) na Jeshi la Polisi.
Amesema katika ziara alizozifanya kwenye mikoa mbalimbali, alitembelea magereza ya Isanga, Msalato (Dodoma), Lindi, Singida na Keko (Dar es Salaam) alikuta nyumba za askari hazina viwango na kama zipo zimechakaa sana.