Wachezaji watatu wametajwa kuwania tuzo ya mchezaji bora wa Afrika na shirikisho la soka barani Afrika (CAF) kwa kupata kura nyingi baada ya kuwepo orodha ya wachezaji kibao walioteuliwa kuwania tuzo hiyo.

Wachezaji hao ni Pierre-Emerick Aubameyang wa Gabon (Borussia Dortmund), Riyad Mahrez wa Algeria (Leicester City) na Sadio Mané wa Senegal (Liverpool) ambao ndiyo watachuana vikali kwenye tuzo hiyo kubwa barani Afrika.

Pierre-Emerick Aubameyang anatetea taji hilo baada ya mwaka jana kuibuka mshindi kwa kumshinda aliyekuwa mpinzani wake mkubwa Yahya Toure wa Manchester City na timu ya taifa ya Ivory Coast.

Mane na Mahrez wanaingia kwa mara ya kwanza kwenye tuzo hizo baada ya kufanya vizuri kwenye klabu zao.

Riyad Mahrez anapewa nafasi kubwa ya kushinda tuzo hiyo baada ya kuiwezesha timu yake ya Leicester City kutwaa kombe la ligi kuu nchini Uingereza pamoja na kufanikiwa kuwa mchezaji bora wa ligi hiyo ya Uingereza.

Katika hatua nyingine shirikisho la soka barani Afrika (CAF) limetoa orodha ya wachezaji wanaowani tuzo ya mchezaji bora wanaocheza ndani ya bara la Afrika ambao ni golikipa wa Uganda Dennis Onyango na Khama Billiat wa Zimbabwe wote wanachezea klabu ya Mamelodi Sundowns na Rainford Kalaba kutoka Zambia na klabu ya TP Mazembe.

Utoaji wa tuzo hizo unatarajia kufanyika nchini Nigeria Januari 5 mwakani kwa kuhudhuriwa na wachezaji mbali mbali pamoja na viongozi wa soka Afrika pamoja na duniani kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *