Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limepiga marufuku kufanyika kwa burudani za watoto maarufu kama disko toto katika kumbi mbalimbali za starehe wakati wa Sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya.

Mkuu wa Operesheni Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Naibu Kamishna wa Polisi, Lucas Mkondya amesema hatua hiyo imefikiwa kutokana na madhara yaliyowahi kutokea siku za nyuma.

Pia amesema Jeshi hilo limejipanga kuhakikisha kunakuwa na ulinzi wa kutosha katika kipindi chote hiki ili wananchi washerehekee sikukuu kwa amani na utulivu kutokana na vitendo vingi vya uhalifu vinavyofanywa na watu wenye nia ovu.

Amesema polisi itaimarisha doria katika maeneo mbalimbali ya jiji ikiwa ni pamoja na kupeleka askari katika kila kanisa ili kuhakikisha ibada zinafanyika katika hali ya amani.

Amewataka wananchi watakaokwenda katika fukwe za bahari kuwa waangalifu na wachukue tahadhari kwa kutowaruhusu watoto kuogelea peke yao na kuepuka kuogelea wakiwa wametumia vileo jambo linaloweza kusababisha madhara.

Pia amewataka watakaotumia magari binafsi kuhakikisha wanayaegesha katika maeneo salama na kuyafunga vizuri huku akiwataka wananchi kutoa taarifa sehemu husika pale wanapoona viashiria vya uhalifu ili wapate msaada.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *