Wanafunzi 10 wa chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wamegharamia masomo yao na kukabidhiwa mkopo wa milioni 10 na taasisi ya Mo Dewji baada ya kukidhi vigezo vya ujasiliamali vya taasisi hiyo.
Mkuu wa Taasisi ya Mo Dewji, Barbara Gonzalez amesema hatua hiyo ni katika kuunga mkono juhudi zinazotoa fursa katika kuleta mafanikio zaidi kwa jamii ya watanzania katika nyanja za afya, elimu na maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Amesema kwa mwaka huu washindi wanne wa shindano la ujasiriamali wamepewa Sh milioni 10 kila mmoja kama mkopo bila riba utakaowezesha kuboresha biashara zao. Mkopo huo unatakiwa kulipwa ndani ya miaka miwili.
Walionufaika na udhamini huo na fani wanazosomea kwenye mabano ni Shabani Maatu kutoka Singida(uhandishi ujenzi), Isack Kuhanga (utengenezaji nguo), Majid Shaban (ualimu) na Thomas Leonard (udaktari) wote kutoka Mwanza.
Wengine ambao wanatoka Kilimanjaro ni Rashid Rashid (uhandisi wa kuchakata kemikali), Alberttina Mella (uhasibu) na Asia Killaghai (sheria), Michael Jordani wa Tanga (uhandisi wa mawasiliano), Pachal Nkololo wa Rukwa(sheria) na Odo Sahini kutoka Mbeya(Molecular Biologya Biotechnology).
Taasisi ya Mo Dewji imeanzishwa mwaka 2014 katika kupunguza umaskini na hali ngumu ya maisha kwa wananchi wa Tanzania kwa kutekeleza mipango ya kusaidia katika maeneo ya elimu, afya na maendeleo ya jamii ambavyo vimekuwa changamoto kwa wananchi wengi.