Jeshi la Polisi limemkamata mtuhumiwa wa utapeli anayejulikana kwa jina la Wilfred Masawe umri miaka (36), mkazi wa Buza, Temeke jijini Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Bulimba, ilieleza kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa akitumia mbinu mbalimbali kutapeli, zikiwemo kujitambulisha kama kiongozi wa serikali kwa kutumia mtandao wa WhatsApp.

Amesema pia alikuwa akieleza kuwa yupo nje ya nchi na kuna tatizo la msiba ambao umetokea nchini na unamhusu na hivyo kutoa maelekezo kwa watendaji wa serikali waweze kusaidia gharama za matibabu hospitalini, gharama za kusafirisha mwili wa marehemu na gharama za mazishi.

Amesema baadhi ya matukio aliyofanikiwa kutapeli ni pamoja na kuwatapeli viongozi wa serikali, wafanyabiashara, mameneja na wakurugenzi wa taasisi za umma, wanasiasa pamoja na waumini wa madhehebu ya dini.

Aidha, matukio yote hayo alikuwa akiyafanya peke yake na alikuwa akiyaendesha kwa mawasiliano ya njia ya ujumbe mfupi (SMS) bila kuzungumza kwa simu.

Bulimba alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha na kuwatahadharisha wananchi wote kuwa makini na mtandao wa matapeli hao na yeyote mwenye taarifa za matapeli aziwasilishe polisi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *