Aliyekuwa mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda ameshinda nafasi ya uenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini.
Shibuda ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama cha Ada Tadea ameshinda nafasi hiyo baada ya kupata jumla ya kula 20 dhidi ya mpinzani wake mwenyekiti wa CCK, Constantine Akitanda ailyepata kura 14.
Mwenyekiti huyo mpya anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Peter Kuga Mziray wa chama APPT Maendeleo kilichofutwa na Msajili wa Vyama vya Siasa.
Baada ya ushindi huo Shibuda amesema atatumia fursa, uzoefu na uwezo alionao kuhakikisha vyama vyote vinakuwa na matumaini ya ushiriki wa kisiasa kupitia heshima ya baraza hilo.
Wengine waliogombea kiti hicho ni Hashim Rungwe (Chaumma), Anna Mghwira (ACT), Fahmy Dovutwa (UPDP), Hassan Kisavya (NRA), na John Cheyo wa UDP ambaye alijitoa.
Baadhi ya vyama vilivyoshiriki katika uchaguzi huo ni Sauti ya Umma (Sau), CUF, CCM, DP, Demokrasia Makini, Jahazi Asilia, Ada-Tadea, CCK na Chadema.
Baraza la Vyama vya Siasa ni chombo kilichoundwa kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa kwa lengo la kuweka jukwaa la kujadiliana masuala yenye masilahi kwa Taifa na uimarishaji wa mfumo wa vyama vingi nchini.