Naibu waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamis Kigwangalla amesema kuwa wizara hiyo inakusudia kuwasilisha muswada wa sheria bungeni mwakani, itakayowalazimisha wahitimu wa udaktari kupangiwa kwenye kituo chochote cha afya.
Dk Hamis Kigwangalla amesema kuwa huenda muswada huo ukawasilishwa rasmi katika Bunge la Februari mwakani.
Dk Kigwangalla aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya sekta ya afya katika kipindi cha mwaka mmoja cha uongozi wa serikali ya awamu ya tano na mikakati ya kuboresha zaidi sekta hiyo katika miaka ijayo.
Alisema endapo sheria hiyo mpya itapitishwa na bunge hilo, inakusudia kubadili muundo mzima wa watumishi wa sekta ya afya.
Naibu waziri huyo, alisema katika mipango na matarajio ya wizara hiyo kwa mwaka ujao wa 2017, pia wanatarajia kutunga sheria ya kuhakikisha kila mtanzania anakuwa na bima ya afya ya lazima.
Alisema katika kutekeleza azma hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja, serikali imefanikiwa kuwakatia bima wazee wote waliopo nchini wanaokadiriwa kufikia takribani milioni mbili na nusu.
Alisema katika sheria hiyo mpya kutakuwa na kifungu cha sheria kitakachobainisha makundi yote yanayotakiwa kukatiwa bima kwa usimamizi wa halmashauri zao.