Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali imeunda Tume kuchunguza taarifa inayoelezea utaratibu uliotumika kumhamisha Faru John kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Sasakwa Black Rhino Sanctuary iliyoko kwenye Hifadhi ya Grumeti Serengeti pamoja na kutafuta kaburi la faru huyo.
Amesema timu hiyo ya wataalamu tayari imeshafika Sasakwa VIP Grumeti kwa ajili ya kutafuta kaburi na kuchukua vinasaba vya masalia ya Faru John na kisha watakwenda kwenye Hifadhi ya Ngorongoro kuchukua vinasaba vya watoto wake na kisha kuvilinganisha na pembe hiyo kubaini kama kweli pembe aliyopelekewa ni ya faru huyo ama la.
Majaliwa aliyasema hayo jana wakati wa majumuisho ya ziara yake ya kikazi mkoani Arusha. Ziara hiyo ililenga kukagua utekelezaji wa shughuli za maendeleo na kuona utoaji wa huduma kwa wananchi.
Waziri mkuu ameema kuwa wakati faru John akiwa V I P Grumeti taarifa zilisema ni mgonjwa na daktari alipompima mara ya kwanza akabaini hakuwa na ugonjwa wowote.
Waziri Mkuu amesema ameiagiza timu hiyo kufanya kazi ya uchunguzi wa taarifa hizo kikamilifu kwa sababu Serikali imetumia fedha nyingi kuwaleta faru hao kutoka nchini Afrika Kusini, ni lazima nyara hizo za Serikali zilindwe kwa manufaa ya Taifa.
Katika kikao cha kukabidhi taarifa kilichofanyika Desemba 9 mwaka huu, akikabidhi pembe za faru huyo mbele ya Waziri Mkuu, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Kupambana na Ujangili wa Wanyamapori, Robert Mande alimweleza kwamba pembe kubwa ya faru John ilikuwa na uzito wa kilo 3.6 na pembe ndogo ilikuwa na uzito wa kilo 2.3.