Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli ametoa msamaha kwa wafungwa 5,678 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira wafungwa 1,340 wataachiwa huru na 4,338 watatumikia kifungo kilichobaki baada ya kupunguziwa moja kwa sita ya vifungo vyao.

Rais ametoa msamaha huo kwa kutumia madaraka aliyopewa chini ya Ibara ya 45 (1) (d) ya Katiba.

Rwegasira imeeleza kuwa wafungwa wote wamepunguziwa vifungo vyao zaidi ya punguzo la kawaida linalotolewa chini ya kifungu 49(1) cha sheria ya Magereza sura ya 58.

Amesema wafungwa waliopewa msamaha huo ni pamoja na wagonjwa wa Ukimwi, Kifua Kikuu (TB) na saratani na ambao wamethibitishwa na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa au wa Wilaya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *