Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka wananchi kuacha tabia ya kuhifadhi fedha nyingi majumbani na badala yake wajenge utamaduni wa kuzipeleka benki.
Ametoa ushauri huo jana wakati akifungua tawi la Benki ya Biashara ya Uchumi lililopo wilayani Karatu, mkoani Arusha akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani hapa.
Akizungumzia kufunguliwa kwa tawi la benki hiyo wilayani Karatu, Waziri Mkuu alisema unaashiria ukuaji wa uchumi wa wilaya hiyo kwa kuwa benki ni kichocheo cha maendeleo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliushauri uongozi wa benki hiyo kuangalia uwezekano wa kupunguza kiasi cha riba wanachokitoza katika mikopo wanayoitoa ili kuwawezesha wananchi kukopa na kupata faida.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo,Wilson Ndesanjo, alisema benki hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo mtaji mdogo, jambo linalowasababisha washindwe kufungua matawi katika mikoa mingine.