Klabu ya Chapecoense ya Brazil ambayo iliwapoteza wachezaji 19 kwenye ajali ya ndege walipokuwa wakielekea kucheza fainali ya Copa Sudamericana imetunukiwa kombe hilo.

Uamuzi huo umechukuliwa na shirikisho la soka la Amerika Kusini, Conmebol kufuatia ombi la wapinzani wa klabu hiyo.

Watu 71, wakiwemo wachezaji 19 na wahudumu wa klabu hiyo, walifariki Jumatatu wakielekea Colombia kwa mechi ya mkondo wa kwanza ya fainali ya kombe hilo.

Atletico Nacional ambao walitakiwa kucheza fainali dhidi ya Chapecoense wameomba klabu hiyo ya Brazil wapewe kombe hilo kama ishara ya kuwakumbuka wachezaji waliopteza maisha kwenye ajali ya ndege.

Pia Atleticoa Nacional wametunukiwa tuzo ya Uchezaji Haki ili kutambua “moyo wao wa amani, kuelewa na kucheza haki”.

Chapecoense watapewa jumla ya $2m (£1.57m) ambazo hukabidhiwa mshindi.

Atletico Nacional nao watapewa $1m (£787,000).

Makamu wa rais wa Chapecoense Ivan Tozzo amesifu uamuzi huo na kuutaja kama “haki”, akihutubia wanahabari jana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *