Waziri Mkuu wa Italia, Matteo Renzi amejiuzulu baada ya kushindwa katika kura ya mabadiliko kuhusu marekebisho ya katiba nchini humo.

Kiongozi huyo alisema anakubali lawama kutokana na matokeo hayo, na kwamba kambi ya La, ambayo ilipinga mageuzi hayo, sasa inafaa kutoa mapendekezo ya mwelekeo kutoka sasa.

Baada ya sehemu kubwa ya kura kuhesabiwa, kambi ya La inaongoza kwa 60% dhidi ya 40% za Ndio.

Waliojitokeza kupiga kura walikuwa takriban 70% ya wapiga kura wote waliojiandikisha, jambo linalotazamwa na wengi kama ishara yao kuonesha kutoridhishwa kwao na waziri mkuu huyo.

Ameeleza kuwa ataitisha mkutano wa baraza la mawaziri baadaye adhuhuri Jumatatu.

Leo atawasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa rais wa Italia baada ya kudumu miaka miwili na nusu.

Renzi amesema mageuzi aliyokuwa amependekeza yangeunguza urasimu mwingi nchini Italia na kuifanya kuwa na ushindani zaidi.

Lakini kura hiyo ya maamuzi ilitazamwa na wengi kama fursa ya kueleza kutofurahishwa kwao na waziri mkuu huyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *