Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ametuma salamu za rambirambi kwa Shirikisho la Mpira la Brazil (CBF), kutokana na vifo vya wachezaji wa timu ya soka Chapecoense Real ya Brazil.
Wachezaji karibu wote wa timu hiyo walikufa katika ajali ya ndege iliyotokea juzi usiku katika milima jirani na Colombia.
Rais wa TFF Malinzi, katika salamu za rambirambi kwa Rais wa (CBF), Lucca Victorelli amesema ajali hiyo iliyoua watu wengi ni tukio la kusikitisha kwenye familia ya soka duniani na limetokea katika kipindi kigumu.
Rais Malinzi ambaye alituma salamu hizo pia kwa mashabiki wa Chapecoense na Jumuiya ya soka na wanafamilia wengine nchini Brazil, amesema: “Mawazo yetu yapo kwa wahanga wa ajali hiyo, familia na jamaa zao.”
Ndege hiyo ilikuwa ikisafiri juzi Jumatatu kutoka Brazil kupitia Bolivia kwenda Colombia ilibeba abiria 81 wakiwamo wafanyakazi na wachezaji wa Chapecoense Real ya Brazil kabla ya kuanguka kwenye milima ya Colombia.
Wachezaji hao wa Chapecoense Real ya Brazil walikuwa wakisafiri kwenda kucheza mechi ya fainali ya michuano ya ubingwa wa Kombe la Amerika ya Kusini (Copa Sud Americana). Walikuwa ni miongoni mwa abiria 81.
Michuano hiyo ni ya pili kwa ukubwa katika Bara la Amerika ya Kusini, iliyotarajiwa kuchezwa jana Jumatano Novemba 30, 2016 ambako Chapecoense Real ingecheza dhidi ya Atletico Nacional ya Colombia katika mchezo wa kwanza wa fainali.
Ndege hiyo ilikuwa imebeba wachezaji wa timu ya Chapecoense Real ya Brazil, awali ilitoa taarifa ya hali ya hatari iliyosababishwa na hitilafu kwenye mfumo wa umeme, na hatimaye kuanguka muda mfupi baadaye karibu na mji wa Medelin.