Raia wa Cuba wameanza kutoa heshima zao za mwisho kwa kiongozi mwanamapinduzi wa taifa hilo Fidel Castro aliyeaga dunia siku ya Ijumaa akiwa na umri wa miaka 90.
Milolongo mirefu imeshuhudiwa katika uwanja wa Revolution Square katika mji mkuu Havana, sehemu ambayo waombolezaji wameweka picha ya kiongozi huyo akiwa ameshika bunduki.
Ilikuwa ni siku ya kwanza ya kipindi cha siku tisa za maombelezi rasmi ya kifo chake.
Siku za maombolezi zitakamilika baada ya majivu ya mwili wake kuzikwa siku ya Jumapili.
Majivu ya Castro yalitazamiwa kuwasilishwa kwa umma katika uwanja wa Revolution Square lakini yamewekwa katika sehemu tofauti.
Wananchi wengi wa Cuba walikuwa katika milolongo hata kabla ya alfajiri kuwadia,ili kuhakikisha wako miongoni mwa watu wa kwanza kutoa heshima zao.